Tupo Kaitaba leo kuikabili Kagera Sugar

Leo saa 10 jioni kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa Kaitaba kuikabili Kagera Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC.

Tutaingia katika mchezo wa leo tukiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa mabao 3-0 tuliyopata kwenye mechi iliyopita dhidi ya Azam FC.

Tunafahamu utakuwa mchezo mgumu kutokana na Kagera kuwa timu bora lakini tumejipanga kuhakikisha tunashinda.

Mgunda atoa neno……

Kaimu Kocha Mkuu, Juma Mgunda amesema maandalizi kuelekea mchezo wa leo yamekamilika.

Mgunda amesema utakuwa mchezo mgumu na tunawaheshimu Kagera kutokana na ubora walionao lakini tumejipanga kuhakikisha tunapata ushindi.

“Maandalizi yamekamilika, tunajua tunaenda kukutana na timu ngumu. Tahadhari zote za kupambana na timu bora zimechukuliwa.”

“Kila timu inayoshiriki Ligi ni bora, na sisi tumejipanga kukabiliana na yoyote na tunawapa heshima sawa huku malengo yetu yakiwa kupata matokeo chanya,” amesema Mgunda.

Kazi aongea kwa niaba ya wachezaji……

Mlinzi wa kati, Hussein Kazi amesema wachezaji wapo kwenye hali nzuri tayari kupambana kwa ajili ya timu kupata ushindi.

“Tunaiheshimu Kagera, na hatuna matokeo mazuri tunapokutana nao hasa katika Uwanja wa Kaitaba lakini tumejipanga kuhakikisha tunashinda,” amesema Kazi.

Tuliwafunga 3-0 Uwanja wa Uhuru

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Disemba 15 mwaka jana tuliibuka na ushindi wa mabao 3-0.

Katika mchezo huo ambao tulifanya mashambulizi mengi mabao yetu yalifungwa na Saido Ntibazonkiza kwa mikwaju wa penati, Sadio Kanoute na nahodha John Bocco.

Babacar arejea mzigoni….

Kiungo mkabaji Babacar Sarr amerejea kikosini baada ya kukosa mechi iliyopita kutokana na kupata majeraha na anategemewa kuwa sehemu ya wachezaji watakao tuwakilisha leo.

Ngoma kuikosa Kagera…..

Kiungo mkabaji Fabrice Ngoma atakosekana kwenye mchezo wa leo kutokana na kutumikia adhabu ya kadi tatu za njano.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER