Kikosi chetu leo saa moja usiku kitashuka katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili Coastal Union kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya NBC ambao tumejipanga kubakisha alama zote tatu nyumbani.
Kwa sasa tumejipanga kuhakikisha tunapata ushindi katika kila mchezo kwa kuwa lengo letu ni kutetea ubingwa wetu ambao tumeutwaa mara nne mfululizo.
Timu iliingia kambini baada ya mchezo wetu wa Jumatano dhidi ya Polisi Tanzania ambao tuliibuka na ushindi bao moja kwa ajili ya maandalizi ya mechi ya leo.
Kocha msaidizi Seleman Matola amesema mapungufu yaliyojitokeza kwenye mechi zilizopita kama kutengeneza nafasi na kushindwa kuzitumia vizuri yameendelea kufanyiwa kazi na anaamini tutapata ushindi mnono.
“Ni kweli tumekuwa hatupati ushindi mnono lakini tumeyaona mapungufu yetu na tumeyafanyia kazi, matumaini yetu ushindi mnono utaanza kupatikana tukianza katika mchezo wa leo,” amesema Matola.
TAARIFA YA KIKOSI
Wachezaji wote walioshiriki katika mchezo uliopita dhidi ya Polisi Tanzania wapo kamili na morali yao ipo juu na yeyote atakayepata nafasi atakuwa tayari kuipigania nembo ya Simba.
TADDEO, SAKHO KUIKOSA COASTAL
Nyota wetu Taddeo Lwanga na Pape Ousmane Sakho hawatakuwa sehemu ya mchezo wa leo kutokana na kutokuwa fiti asilimia mia ingawa hali zao zinaendelea vizuri.
Mshambuliaji Chris Mugalu bado anaendelea kuuguza jeraha la mguu na anatarajia kurejea uwanjani wiki chache zijazo sababu afya yake inazidi kuimarika.