Tunazitaka alama tatu za Biashara

Timu yetu leo itashuka katika Uwanja wa Karume mkoani Mara saa 10 jioni kucheza mechi ya kwanza ya Ligi Kuu dhidi ya Biashara United.

Katika mchezo wa leo tunahitaji kupata alama tatu muhimu ili kurudisha imani kwa mashabiki wetu na kupunguza presha kwa wachezaji hasa baada ya kupoteza mechi ya Ngao ya Jamii Jumapili iliyopita.

Kuelekea mchezo wa leo Kocha Msaidizi Seleman Matola ameweka wazi kuwa utakuwa mgumu kutokana na uimara wa wapinzani hasa wanapokuwa nyumbani ingawa tumejipanga kuwakabili kwa hali yoyote.

Matola amewataka mashabiki wetu kujitokeza kwa wingi uwanjani kuwapa hamasa wachezaji huku akiahidi kupambana hadi mwisho kuhakikisha tunaondoka na alama zote tatu ugenini.

“Maandalizi ya mchezo yamekamilika na wachezaji wote wapo kwenye hali nzuri na lengo letu ni moja kushinda ili kuanza ligi vizuri kikubwa tunawaomba mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi,” amesema Matola.

TAARIFA YA KIKOSI

Kikosi kimewasili hapa mkoani Mara jana kikitokea jijini Mwanza kikiwa na wachezaji 23 ambao wote wapo tayari kwa mchezo wa leo.

KANOUTE, ONYANGO, MKUDE KUKOSEKANA

Nyota wetu Sadio Kanoute na Joash Onyango hawakusafiri na timu kutokana na kupata majeraha katika mchezo uliopita wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga.

Jonas Mkude alipatwa na msiba ambapo alikwenda kushiriki mazishi ya mtoto wake mkoani Morogoro hivyo alichelewa katika maandalizi ya mchezo huku Ibrahim Ajibu na kiungo Abdulsamad Kassim wakibaki Dar es Salaam.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER