Kikosi chetu leo kitashuka katika Uwanja wa Kimataifa wa Tripoli kucheza na Al Ahli Tripoli katika mchezo wa hatua ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika ambao utapigwa saa mbili usiku kwa saa za Tanzania.
Baada ya miaka kadhaa ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa kwa sasa tumeangukia huku Kombe la Shirikisho Afrika.
Kikosi kipo kwenye hali nzuri na tunajua tunakutana na timu imara lakini tupo tayari kuwakabili na kupata matokeo chanya.
Kocha Fadlu afunguka…..
Kocha Mkuu Fadlu Davids amesema kikosi kimepata siku mbili ya kufanya mazoezi nchini Libya ambazo zimewasaidia kuzoea hali ya hewa na wamefanya katika Uwanja tutakaocheza kesho.
Akizungumzia mchezo wenyewe Fadlu amesema utakuwa mgumu hasa kutokana na Tripoli kufanya usajili wa wachezaji wengi bora na wenye uzoefu wa michuano hii.
“Tunafahamu kesho uwanja utakuwa na mashabiki wengi ambao watakuja kuipa sapoti timu yao lakini tumewaandaa wachezaji kukabiliana na hilo,” amesema Kocha Fadlu.
Zimbwe Jr azungumzia mchezo……
Nahodha wa timu, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ amesema wachezaji wapo tayari kufuata maelekezo watakayopewa na walimu ili kukamilisha mipango ya timu.
Zimbwe Jr amesema tunafahamu utakuwa mchezo mgumu na tunawaheshimu wapinzani wetu hasa ukizingatia tupo ugenini.
“Kwa upande wetu wachezaji tupo kwenye hali nzuri kwa ajili ya mchezo wa kesho, kila atayepata nafasi atakuwa tayari kuipigania timu kupata matokeo chanya,” amesema Zimbwe Jr.
Nyota nane ndio wenyeji….
Katika kikosi cha wachezaji 22 tuliosafiri nao ni nyota tisa tu ambao ni walikuwepo kwenye timu iliyoshiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika huku 13 wakiwa ni wageni.
Nyota waliokuwa msimu uliopita ni Aishi Manula, Ally Salim, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’, Che Malone, Fabrice Ngoma, Kibu Denis na Edwin Balua.