Tunataka kuvunja rekodi yao leo

Leo saa 11 jioni kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili Yanga kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya NBC ya mzunguko wa pili.

Tutaingia katika mchezo wa leo tukiwa na lengo moja kupata alama tatu na kuwa timu ya kwanza msimu huu kuvunja rekodi ya kutofungwa ya vinara hao.

Hali za wachezaji ni vizuri wamefanya mazoezi ya mwisho jana asubuhi na hakuna ambaye amepata majeraha yatakayomfanya kuukosa mchezo.

PABLO HANA HATA WASIWASI

Kocha Mkuu Pablo Franco ameweka wazi kuwa hana wasiwasi wala presha kuelekea mchezo wa leo ambapo amesema kila kitu kimekaa sawa.

Pablo amesema tuna wachezaji bora wenye uzoefu wa kucheza mechi kubwa zenye presha hivyo haitakuwa tofauti ingawa ni Derby na inavuta hisia za wengi.

Pablo ameongeza kuwa mchezo utakuwa mgumu lakini tumejiandaa kuhakikisha tunapata alama tatu ili kupunguza tofauti na kuwapa presha wanaoongoza.

“Hatuna presha yoyote kuelekea mchezo wa leo. Simba ni timu kubwa na ina wachezaji bora pia inacheza vizuri zaidi yao na inapenda kucheza mechi kubwa pia. Tuna fahamu utakuwa mchezo mgumu lakini tumejipanga vizuri,” amesema Pablo.

KAPOMBE: NGUVU ZA SHIRIKISHO AFRIKA TUMEZIHAMISHIA KWENYE LIGI

Mlinzi wa kulia Shomari Kapombe amesema baada ya kutolewa katika Michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika sasa tumeelekeza nguvu katika michuano ya Ligi Kuu tukianza na mchezo wa leo.

Kapombe amesema bila kuangalia tofauti ya pointi iliyopo baina yetu na vinara tutaendelea kupambana hadi mwisho wa msimu tuangalie tumepata nini.

“Baada ya kutolewa Shirikisho Afrika sisi kama wachezaji tulikaa na kupanga kuhusu mchezo huu mkubwa ambao unavuta hisia kubwa, mashabiki wetu hawakujisikia vizuri na malengo ni kuwafurahisha kwa ushindi dhidi ya Yanga kesho,” amesema Kapombe.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER