Ijumaa ya Machi 29 kikosi chetu kitacheza mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly mtanange utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa saa tatu usiku.
Mchezo wa marudiano utapigwa Aprili 5 jijini Cairo nchini Misri na mshindi wa jumla atasonga mbele na kutinga nusu fainali.
Hii ni Robo fainali yetu ya nne ya Ligi ya Mabingwa katika miaka mitano tangu mwaka 2019.
2020 ndio mwaka pekee ambao hatujatinga robo fainali ya michuano hii katika miaka hii mitano.
Hizi hapa mechi zetu tatu za hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
1. Aprili 6, 2019
Simba 0 -0 Tp mazembe
Mechi ya marudiano Aprili 13, 2019
Tp mazembe 4 -1 Simba
2. Mei 15, 2021
Kaizer Chiefs 4-0 Simba
Mechi ya marudiano Mei 22, 2021
Simba 3 -0 Kaizer Chiefs
3. Aprili 22, 2023
Simba 1 -0 Wydad Casablanca
Mechi ya marudiano Aprili 28, 2023
Wydad 1-0 Simba
Penati 4-3
Malengo yetu….
Tutaingia katika mchezo huo tukiwa na kiu kubwa ya kuvuka hatua ya robo fainali na kutinga nusu fainali ya michuano hii mikubwa barani Afrika.
Tunafahamu Al Ahly ni timu yenye historia kubwa barani Afrika kwa kuchukua taji hili mara nyingi lakini safari hii tunajidhatiti ili tuvuke hatua hii.
Benchikha ana uzoefu na mechi hizi…
Kocha Mkuu Abdelhak Benchikha yeye sio mgeni wa mechi kubwa na zenye presha kama hizi.
Msimu uliopita aliiwezesha USM Alger ya Algeria kuchukua taji la Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuifunga Yanga ya Tanzania.
Benchikha akiwa na USM Alger alichukua taji la Super Cup kwa kuifunga Al Ahly msimu uliopita.
Chama aizungumzia mechi hii……
Kiungo mshambuliaji Clatous Chama amesema itakuwa mechi ngumu na tunaiheshimu Al Ahly lakini hatuwaogopi na tupo tayari kupambana nao.
Chama amesema katika miaka mitano tuliyofika hatua hii tumejifunza mambo mengi tunajua jinsi ya kukabiliana na miamba hiyo.
“Tunaiheshimu Al Ahly lakini hatuwaogopi, tumejifunza mambo mengi na tupo tayari kuwakabili, tunahitaji nasi kuvuka na kuingia nusu fainali,” amesema Chama.