Tunaitaka Nusu Fainali ya CAFCC Leo

Leo saa 10 jioni kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili Al Masry katika mchezo wa marudiano wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAFCC).

Tutaingia katika mchezo wa leo kwa dhamira moja tu ya kuhakikisha tunashinda na kutinga nusu fainali ya michuano hii ambayo tumeisubiri kwa miaka mingi.

Tunafahamu tuna kazi kubwa ya kufanya ili kufanikisha malengo yetu hasa ukizingatia tumetoka kupoteza mchezo wa mkondo wa kwanza ugenini.

Fadlu awafungia kazi washambuliaji…….

Kocha Mkuu, Fadlu Davids amesema katika kipindi cha wiki nzima cha maandalizi ya mchezo huu amewasisitiza wachezaji kuhakikisha wanafunga kila wanapopata nafasi.

Fadlu amesema tunatakiwa kupata ushindi wa mabao matatu ili kufuzu nusu fainali lakini amewaandaa wachezaji kuhakikisha wanafunga zaidi ya manne ili kucheza bila presha.

“Tunahitaji mabao matatu ili kufuzu nusu fainali na hii wiki nzima tumefanya mazoezi walau tufunge mabao zaidi ya manne na sio matatu pekee,” amesema Fadlu.

Wachezaji wapo tayari kwa vita ya dakika 90……..

Akizungumza kwa niaba ya wachezaji nahodha wa timu, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ amesema kila mmoja yupo tayari kuhakikisha anakuwa sehemu ya kikosi kilichoandika historia ya kuipeleka timu nusu fainali.

“Tukiwa na wachezaji wageni tunawaambia kuwa kufika robo fainali sio mafanikio kwakuwa sisi tushafanya mara nyingi ila wanatakiwa kuhakikisha tunasaidiana kutoka hapa na kuifikisha timu nusu fainali,” amesema Zimbwe Jr.

Ni mechi ya kisasi…….

Mchezo wa leo ni kisasi kwakuwa tayari tumepoteza mechi ya kwanza ugenini kwa mabao 2-0 hivyo tunahitaji kupindua matokeo ili tuweze kufuzu na kutinga nusu fainali.

Pia mwaka 2018 katika hatua ya awali ya michuano hii tulikutana na Al Masry na kutoka sare ya mabao 2-2 nyumbani na sare 0-0 ugenini hivyo hawajawahi kuonja kipigo kutoka kwa kwetu na Leo ndio siku yao.

Historia inatubeba kwa Mkapa……..

Katika Uwanja wa Benjamin Mkapa hakuna kitu ambacho hatujawahi kukifanya. Kuwa nyuma kwa mabao mawili hakutupi presha kwakuwa tunaimani tunaweza kupata zaidi ya hayo na kufuzu nusu fainali.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER