Kikosi chetu leo saa 10 jioni kitashuka katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kufungua pazia la mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya NBC kwa kucheza na Geita Gold.
Maandalizi ya mchezo yamekamilika, kikosi kiliwasili juzi jijini hapa na jana kimefanya mazoezi ya mwisho katika kujiweka sawa kabla ya mechi ya leo.
Tutaingia katika mchezo wa leo kwa kuiheshimu Geita Gold na tunajua ni timu nzuri inacheza nyumbani kwahiyo tumechukua tahadhari zote na lengo ni kuhakikisha tunapata pointi zote tatu.
KAULI YA KOCHA MGUNDA
Kocha mkuu, Juma Mgunda amesema kikosi kipo katika hali nzuri wachezaji wote 24 ambapo tumesafiri nao wapo kamili kupambana kuhakikisha pointi tatu zinapatikana CCM Kirumba leo.
Mgunda ameongeza kuwa tunaiheshimu Geita na tunategemea kupata upinzani mkubwa lakini tumejidhatiti kuhakikisha tunashinda.
“Maandalizi yamekamilika na wachezaji wapo kwenye hali nzuri, tunaiheshimu Geita na tunategemea kupata ushindani mkubwa lakini tupo tayari kuwakabili,” amesema Mgunda.
ZIMBWE JR: WACHEZAJI TUPO TAYARI KWA GEITA
Kwa upande wake, nahodha msaidizi Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ amesema wachezaji wapo tayari kufuata maelekezo ya benchi la ufundi ili kuhakikisha pointi tatu zinapatikana leo.
“Sisi kama wachezaji tupo tayari kufuata maelekezo tutakayopewa na walimu wetu ili kushinda. Tunategemea kupata upinzani mkubwa kutoka kwa Geita na tunawaheshimu lakini tumejipanga kuhakikisha tunashinda,” amesema Zimbwe Jr.
TULIWAFUNGA 3-0 KWA MKAPA
Mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Agosti 17 tuliibuka na ushindi mabao 3-0 yaliyofungwa na Augustine Okrah, Moses Phiri na Clatous Chama kwa mkwaju wa penati.