Tunafunga mwaka kwa Mkapa leo

Kikosi chetu leo kitashuka Uwanja wa Benjamin Mkapa kucheza na Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC ambao utakuwa wa mwisho kwa mwaka huu.

Baada ya mchezo wa leo hatatukuwa na mchezo mwingine hadi 2023 ambapo tutaanzia Visiwani Zanzibar kwenye Michuano ya Kombe la Mapinduzi.

Tunaingia kwenye mchezo wa leo tukiwa na lengo moja la kuwafurahisha mashabiki kwa kuonyesha kandanda safi pamoja na kupata alama tatu.

MGUNDA: KIKOSI KIPO TAYARI

Kocha Mkuu Juma Mgunda amesema maandalizi ya mchezo yamekamilika na kikosi kipo kwenye hali nzuri, morali ya wachezaji ipo juu tayari kuipigania timu.

Mgunda ameongeza kuwa mchezo utakuwa mgumu kwani tunaiheshimu Prisons lakini tumejipanga kikamilifu kuhakikisha tunafunga mwaka kwa ushindi pamoja na kuonyesha kandanda safi.

“Maandalizi yote ya mchezo yamekamilika wachezaji wapo kwenye hali nzuri, tunategemea kupata upinzani mkubwa lakini tupo tayari kupambana,” amesema Mgunda.

GADIEL ATOA NENO

Kwa niaba ya wachezaji mlinzi wa kushoto, Gadiel Michael amesema kila kitu sawa kwa upande wao na yeyote atakayepata nafasi ya kucheza atakuwa tayari kuitumikia timu.

“Sisi wachezaji tupo tayari kwa mchezo, morali zipo juu. Tunawaheshimu Prisons ni timu nzuri lakini tumejipanga kuhakikisha tunapata pointi zote,” amesema Gadiel.

AHMED AWAITA MASHABIKI KWA MKAPA

Meneja Habari na Mawasiliano, Ahmed Ally amewaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi uwanjani kwakuwa ndio mchezo wa mwisho katika mwaka 2022 na tupo nyumbani hivyo itakuwa vizuri kushangilia ushindi pamoja.

“Tunahitaji kuweka rekodi ya mapato kwenye mchezo wa leo na kuondoa dhana kuwa ili kujaza uwanja lazima tucheze na timu kubwa za Dar es Salaam.

“Mashabiki leo ndiyo siku yetu kubwa ya kukutana uwanjani kuwashangilia wachezaji wetu na kufunga mwaka, tunajua wachezaji watatulipa kwa ushindi,” amesema Ahmed.

TULIWAFUNGA BAO MOJA SOKOINE

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa ligi uliopigwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Septemba 14 tulifanikiwa kupata ushindi wa bao moja.

Kwenye mchezo huo bao letu lilifungwa dakika za majeruhi na kiungo mkabaji Jonas Mkude.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER