Tunaendelea tulipoishia

Baada ya mapumziko ya wiki mbili kupisha mechi za kufuzu fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) kikosi chetu leo kitashuka katika Uwanja wa Benjamin Mkapa saa moja usiku kuikabili KMC kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya NBC.

Tutaingia kwenye mchezo wa leo tukiwa na alama sita baada ya kucheza mechi mbili tukifunga mabao matano tukiwa hatujaruhusu kufungwa.

Tumekuwa na rekodi bora kila tunapokutana na KMC lakini hatutaingia uwanjani kwa historia bali tutapambana kutafuta alama tatu.

MATOLA: HATUTAICHUKULIA POA KMC

Kaimu Kocha Mkuu Seleman Matola ameweka wazi mchezo utakuwa mgumu na tutaingia kwa kuwaheshimu lakini lengo letu ni kuhakikisha tunashinda.

Matola amesema wachezaji wapo kwenye hali nzuri, morali ipo juu na wale waliokuwa kwenye majukumu ya timu ya taifa tayari wamejiunga na wenzao.

“Mchezo utakuwa mgumu, tunaiheshimu KMC ni timu nzuri, inatupa changamoto kubwa kila tunapokutana nao lakini tumejipanga kuhakikisha tunabaki na alama zote tatu,” amesema Matola.

ZIMBWE JR AWAITA MASHABIKI KWA MKAPA

Nahodha Msaidizi Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ amewaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi katika mchezo wa leo ili kuwapa sapoti wachezaji ili kuhakikisha tunapata ushindi.

Zimbwe Jr amesema kwa upande wao wachezaji wapo tayari kwa mchezo na watafuata maelekezo watakayopewa na walimu ili kufanikisha malengo ya kuchukua alama tatu.

“Sisi wachezaji tupo kamili kwa mchezo kila mmoja ambaye atapangwa atakuwa tayari kupambana kuipigania timu, morali ipo juu na tunajua mchezo utakuwa mgumu lakini tumejipanga kushinda,” amesema Zimbwe Jr.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER