Kikosi chetu leo saa nne usiku kitashuka katika Uwanja wa Felix – Houphouet kuikabili ASEC Mimosas katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mchezo wa leo ni muhimu kwetu kupata alama tatu ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya robo fainali.
Tunahitaji kupata ushindi ambao utatufanya kufikisha pointi nane na kuzidi kuwasogelea vinara ASEC wenye alama 10 ili mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi ambao tutacheza nyumbani iwe ni faida kwetu.
Benchikha atoa neno…..
Kocha Mkuu Abdelhak Benchikha amesema pamoja na umuhimu na ukubwa wa mchezo wa leo lakini hatutacheza kwa presha wala hofu na tutaingia uwanjani kwa lengo la kutafuta pointi tatu.
Benchikha amesema utakuwa mchezo mgumu hasa kwakuwa tunacheza ugenini lakini tumejiandaa kuhakikisha tunapata matokeo ya ushindi.
“Tunafahamu utakuwa mchezo mgumu, tunahitaji kushinda ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya robo fainali, malengo yetu ni kupata pointi tatu,” amesema Benchikha.
Fred afurahia kucheza ardhi ya nyumbani….
Mshambuliaji, Fred Michael Kouablan amesema anajisikia fahari kucheza katika ardhi ya nyumbani kwao Ivory Coast kwakuwa familia na ndugu zake watakuja uwanjani kumtazama.
“Inafurahisha kucheza katika ardhi ya nyumbani, ndugu pamoja na familia wanakuja uwanjani kukupa sapoti. Sisi kama wachezaji tupo tayari kupambana ili kuisaidia timu kupata ushindi,” amesema Fred.
Hali ya kikosi……
Wachezaji wote 22 wapo kwenye hali nzuri na kila atakyepata nafasi ya kucheza atakuwa tayari kuipigania timu.
Morali zao zipo juu na wote wamefanya mazoezi ya mwisho jana usiku tayari kwa mchezo wa leo.