Saa 10:15 jioni kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa KMC kuikabili Tabora United kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 202/25.
Mchezo wa leo tumeupa umuhimu mkubwa na malengo yetu ni kuhakikisha tunapata ushindi ili kujiweka sawa kwenye harakati za kupigania taji la ubingwa.
Wachezaji wapo kwenye hali nzuri na morali zao juu na wapo tayari kwa mchezo wa leo.
Kocha Fadlu afunguka…….
Kocha Mkuu, Fadlu Davids amesema kikosi chetu kimepata wiki sita za mazoezi pamoja na kucheza mechi kadhaa za kirafiki pamoja zile za Ngao ya Jamii hivyo kipo tayari kwa Ligi Kuu.
Kocha Fadlu ameongeza kuwa malengo yetu ni kuhakikisha tunaanza vizuri ligi kwa kuanza na ushindi dhidi ya Tabora leo.
“Timu ipo tayari kwa kuanza Ligi Kuu, kikosi chetu kipo kwenye umbo bora la kiushindani na mawasiliano ndani ya uwanjani yameendelea kuimarika,” amesema Kocha Fadlu.
Abel aongea kwa niaba ya wachezaji…..
Mlinda mlango, Hussein Abel amesema wao kama wachezaji wamejipanga kuhakikisha tunafanya vizuri kwenye mechi ya leo na wapo tayari kuwapa furaha Wanasimba.
“Sisi kama wachezaji tupo tayari, tunaamini utakuwa mchezo mgumu lakini tumejipanga kuhakikisha tunashinda,” amesema Abel.
Mara ya mwisho tuliwafunga….
Mchezo wa mwisho tuliokutana na Tabora United msimu uliopita uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Mei 6 tuliibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Katika mchezo huo mabao yetu yalifungwa na Sadio Kanoute na Edwin Balua.