Tunaanza Mzunguko wa pili wa Ligi dhidi ya Tabora Leo

Leo saa 10 jioni kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi mkoani Tabora kuikabili Tabora United katika mchezo wa kwanza wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya NBC.

Tutaingia kwenye mchezo wa leo tukiwa na kumbukumbu nzuri kutokana na ushindi mnono wa mabao 6-0 tuliopata wiki iliyopita dhidi ya Kilimanjaro Wonders kwenye mchezo wa CRDB Federation Cup.

Tunafahamu utakuwa mchezo mgumu lakini kama ilivyo kawaida tutaingia uwanjani kwa lengo la kutafuta alama tatu muhimu ugenini.

Hiki ndicho alichosema Fadlu kuhusu mchezo

Kocha Mkuu, Fadlu Davids amesema mchezo wa leo utakuwa tofauti na ule tuliocheza mzunguko wa kwanza kwakuwa wapinzani wamejipanga vizuri na hawatapenda kupoteza tena wakiwa nyumbani lakini tupo tayari kuwakabili.

“Tumejipanga kwa ajili ya mechi zote za mzunguko wa pili tukianza leo dhidi ya Tabora. Tunategemea kupata upinzani mkubwa lakini tumejipanga kucheza aina ya soka letu ingawa itategemea na hali ya Uwanja utakavyokuwa,” amesema Fadlu.

Wawili kuikosa Tabora

Kocha Mkuu Fadlu Davids ameweka wazi kuwa katika mchezo wa leo tutakosa huduma ya wachezaji wawili kiungo, Awesu Awesu na mlinda mlango, Aishi Manula.

“Kiungo mshambuliaji, Awesu Awesu ambaye alipata maumivu kwenye mechi dhidi ya Kilimanjaro Wonders hatakuwa sehemu ya mchezo pamoja na mlinda mlango Aishi Manula anayesumbulia na mafua lakini wengine wote wapo tayari,” amesema Fadlu.

Ally Salim afunguka kuhusu ahadi waliyoahidiwa Tabora

Mlinda mlango, Ally Salim amesema wachezaji hawatishiki na ahadi waliyopewa Tabora endapo watapata ushindi dhidi yetu badala yake wamejipanga kufuata maelekezo ya walimu ili kutimiza malengo ya kuondoka na pointi zote tatu.

“Sisi tutaingia uwanjani kucheza kwa kufuata maelekezo ya walimu wetu, kuhusu ahadi walizoaahidiwa wapinzani wetu hazituumizi kichwa na wala hazitatutoa mchezoni badala yake tutafuata mbinu zetu,” amesema Salim.

Tuliwafunga Mzunguko wa Kwanza

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi uliopigwa Agosti, 18, 2024 katika Uwanja wa KMC Complex tuliibuka na ushindi wa mabao 3-0.

Mabao hayo yalifungwa na mlinzi Che Fondoh Malone, Valentino Mashaka na Awesu Awesu.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER