Tuna kibarua cha pili Uhuru Leo

Saa 10 jioni kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam kuikabili Dodoma Jiji kwenye mchezo wa pili wa Ligi Kuu ya NBC.

Tunaingia kwenye mchezo wa leo tukiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa mabao 4-2 tuliopata katika mechi ya kwanza ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar.

Tunafahamu tutapata upinzani mkubwa kwa Dodoma Jiji kutokana na ubora wa kikosi chao lakini tupo tayari kupigania pointi tatu za nyumbani.

Robertinho: Tunaiheshimu Dodoma……..

Kocha Mkuu, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amesema tutaingia kwa kuwaheshimu wapinzani kwakuwa tunafahamu ni timu bora.

Robertinho amesema pamoja na kuwaheshimu wapinzani lakini tumejipanga kucheza soka safi na kupambana kupata pointi tatu za nyumbani.

“Kikosi kipo tayari kwa ajili ya mchezo. Wachezaji wapo kwenye hali nzuri kuhakikisha tunapata alama tatu.

“Tunawaheshimu Dodoma lakini tutaingia uwanjani kwa lengo la kuhakikisha tunacheza soka safi na kushinda,” amesema Robertinho.

Abdallah, Ntibazonkiza wazungumzia mechi….

Nyota, Abdallah Hamis na Saido Ntibazonkiza wamefunguka kuwa licha yakuwa kesho tunacheza katika ardhi ya Dar es Salaam mchezo dhidi ya Dodoma Jiji utakuwa mgumu.

Abdallah amesema haitakuwa mechi rahisi na tutapata upinzani mkubwa kutoka kwa Dodoma lakini Simba ni timu kubwa na imekamilika kila idara hivyo uwezekano wa ushindi ni mnono upo.

Ntibazonkiza yeye amesema mara zote kila timu inapokutana nasi lazima mchezo uwe mgumu lakini tupo tayari kwa changamoto yoyote itakayotokea.

Tutaendelea kuwakosa Inonga, Kramo…..

Kwenye mchezo wa leo tutawakosa nyota wetu Henock Inonga na Aubin Kramo ambao ni majeruhi.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER