Tuna jambo letu na Mbeya City kwa Mkapa leo

Baada ya mapumziko ya wiki mbili kupisha mechi za kufuzu michuano ya AFCON kikosi chetu leo kitashuka katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili Mbeya City kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya NBC utakaoanza saa moja usiku.

Tunashuka katika mchezo wa leo tukiwa na lengo la kuhakikisha tunachukua alama zote tatu na kuonyesha kandanda safi lengo likiwa ni kuwapa furaha mashabiki wetu.

Tunajua mchezo utakuwa mgumu kutokana na ligi kuelekea ukingoni na mara zote City wamekuwa wakitupa upinzani mkubwa lakini tupo tayari kupambana kubakisha alama zote tatu nyumbani.

Kaimu Kocha Mkuu Seleman Matola, amesema baada ya kuukosa rasmi ubingwa lengo lililobaki ni kuhakikisha tunamaliza ligi kwa heshima kwa kupata matokeo.

Matola amesema Mbeya City ni timu nzuri inacheza soka safi lakini tumejipanga kuhakikisha tunawadhibiti ili kupata ushindi.

“Tuko tayari kwa mchezo wa leo, wachezaji wapo kwenye hali nzuri maandalizi yamekamilika na tuna imani tutapata alama zote tatu. Tumeukosa ubingwa lakini tunataka kumaliza ligi kwa heshima.

“Tunaiheshimu Mbeya City, inatupa ushindani mkubwa tukikutana nayo lakini tupo tayari kukabiliana nao kulingana na maandalizi tuliyofanya,” amesema Matola.

KIKOSI KIPO TAYARI

Kikosi chetu kipo kamili wachezaji waliokuwa katika majukumu ya timu za taifa wamerejea na wamejiunga na wenzao tayari kwa mchezo wa leo.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER