Tumezifuata pointi tatu kwa Mtibwa

Leo saa 10 jioni kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa Manungu mkoani Morogoro kuikabili Mtibwa Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC ambao tumelenga kuondoka na alama zote tatu.

Kikosi kiko kamili na jana jioni kilifanya mazoezi ya mwisho katika Uwanja wa Highland kujiandaa na mchezo huo ambao tunataraji utakuwa mgumu.

Nyota wetu wote tuliosafiri nao wako kwenye hali nzuri kimwili na kiakili na yoyote atakayepata nafasi ya kucheza kutokana na matakwa ya benchi la ufundi atakuwa tayari kuipigania timu.

ALICHOSEMA KOCHA PABLO

Kocha Mkuu Pablo Franco, amesema licha ya Uwanja wa Manungu kutokuwa rafiki sana kwa aina ya soka tunalocheza lakini tumejipanga kutandaza kandanda safi la kuwafurahisha mashabiki wetu.

“Jana jioni tumefanya mazoezi ya mwisho kabla ya mchezo wa leo, wachezaji wapo katika hali nzuri. Tunataraji kucheza soka safi ingawa tunajua uwanja hautakuwa rafiki kwetu,” amesema Pablo.

MANULA NAYE ATOA NENO

Mlinda mlango namba moja, Aishi Manula ameweka wazi kuwa mchezo utakuwa mgumu sababu mara zote timu ndogo ikikutana na kubwa lazima ikaze ingawa hata hivyo tumajipanga kwa kila kitu.

“Tunaiheshimu Mtibwa ni timu nzuri na imekuwa ikitupa ushindani mkubwa kila tukikutana nao, tunajua wapo katika uwanja wa nyumbani lakini Simba ni timu kubwa na inaweza kushinda popote,” amesema Manula.

MKUDE, KIBU KUIKOSA MTIBWA

Nyota wetu, Jonas Mkude na Kibu Denis hawatakuwa sehemu ya mchezo wa leo kutokana na kuendelea kuuguza majeraha na wamebaki jijini Dar es Salaam.

Wawili hao walipata maumivu katika mchezo wetu uliopita dhidi ya Mbeya City ambapo wanaendelea vizuri kwa sasa.

SHARE :
Facebook
Twitter

One Response

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER