Kikosi chetu kimetolewa na Mamelodi Sundowns katika mchezo wa Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kupoteza kwa bao moja.
Tulianza mchezo huo kwa kasi kwa kuliandama lango la Mamelodi lakini tulikosa umakini wa kutumia nafasi tulizotengeneza.
Kocha Charles Lukula alifanya mabadiliko ya mapema ya kumtoa S’arrive Lobo na kumuingiza Pambani Kuzoya dakika ya 30 ili kuongeza mashambulizi pamoja na kuzuia.
Boitumelo Rabale aliwapatia Mamelodi bao hilo dakika ya 76 kwa mguu wa kushoto akiwa nje kidogo ya 18 akimalizia mpira wa krosi kutoka upande wa kushoto.
Baada ya kufungwa bao hilo Kocha Lukula alimtoa Koku Kipanga, Opa Clement na Diana Mnali na kuwaingiza Olaiya Barakati, Philomena Abakah na Topister Situma ili kuongeza nguvu.
Kufuatia kushindwa kutinga fainali sasa tunasubiri kucheza mechi ya kutafuta mshindi wa tatu na atakayepoteza mchezo wa nusu fainali ya pili itakayopigwa kesho.