Mchezo wetu wa kwanza wa kirafiki dhidi ya Zira FC uliopigwa Uwanja wa Vonresort umemalizika kwa sare ya kufungana bao moja.
Mchezo ulianza kwa kasi katika dakika 15 za kwanza huku timu zote zikishambuliana kwa zamu lakini hakuna iliyopata bao.
Dakika ya 19 Zira walipata penati baada ya mchezaji wao kufanyiwa madhambi ndani ya 18 lakini mkwaju huo uliopigwa na Filip Pahtmann uliokolewa na mlinda mlango Ally Salim.
Kibu Denis alitupatia bao la kwanza dakika ya 33 kwa shuti kali baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Said Ntibazonkiza.
Baada ya bao hilo Zira waliliandama lango letu na kufanya mashambulizi kadhaa lakini ukuta wetu ulikuwa imara.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku kila timu ikiwa na dhamira ya kutafuta bao lakini umakini wa kutumia nafasi zilizopatikana ulipungua.
Zira walipata bao la kusawazisha kupitia Rustam Ahmadzade dakika ya 63 baada ya kuunganisha krosi ya Fuad Bayramov.
Kocha Mkuu Roberto Oliviera ‘Robertinho’ alifanya mabadiliko ya kuwatoa Willy Onana, Aubin Kramo, na Sadio Kanoute na kuwaingiza Clatous Chama, John Bocco, Fabrice Ngoma na Israel Patrick.