Menejimeti ya Klabu kwa kushirikiana na Mo Dewji Foundation tumetembelea Shule ya Msingi Buguruni Viziwi na kutoa msaada wa vifaa vya Michezo.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu, Ahmed Ally amesema Simba ni timu ambayo ina mashabiki wa kila aina kutoka kila sehemu ndio maana kila mwaka tunawafikia hadi wenye uhitaji.
Ahmed amesema leo tumetoa vifaa vya michezo kwa shule saba za watoto wenye ulemavu vyenye thamani ya Shilingi milioni nane.
“Imekuwa ni desturi yetu kila mwaka kuelekea Tamasha Simba Day ya kutoa misaada kwa wenye uhitaji ili nao wao wajisikie ni sehemu ya Simba.”
“Hapa Buguruni ni kama mfano lakini tumegawa vifaa vya michezo kwa shule saba zikiwemo Mugabe, Tuangoma, Chalinze ili na watoto wetu nao wajione ni sehemu ya timu hii,” amesema Ahmed.
Aidha Ahmed ametoa wito kwa Wanasimba wote nchi nzima “Uongozi wa klabu kwa kushirikiana na Mo Dewji Foundation hauwezi kuwafikia Wanasimba wote kwahiyo mkiwa kama Tawi au Kundi kama mnayo nafasi niwasisitize muende mkatoe kwa wenye uhitaji.”
Wiki hii kuelekea kilele cha Simba Day huwa kuna matukio ya shughuli mbalimbali za kijamii kama jana tulikuwa na zoezi la uchangiaji damu nchi nzima.