Tumetinga Robo Fainali Shirikisho kibabe

Timu yetu imefanikiwa kutinga robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika kwa kushindo baada ya kuichakaza bila huruma US Gendarmerie mabao 4-0 katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Tulianza mchezo kwa kasi na kuliandama lango la Gandarmerie lakini wachezaji wetu walikosa utulivu katika eneo la mwisho la wapinzani ambapo tulipoteza nafasi ambazo zingetufanya kwenda mapumziko tukiwa mbele.

Sadio Kanoute alitupatia bao la kwanza dakika ya 63 kwa shuti kali la chini chini akiwa ndani ya 18 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Bernard Morrison.

Mlinzi wa kushoto na nahodha msaidizi Mohamed Hussein kushindwa kuendelea na mchezo baada ya kuumia nyama za paja nafasi yake ikachukuliwa na Israel Patrick.

Chris Mugalu aliongeza la pili dakika ya 68 akimalizia kazi nzuri iliyofanywa na Morrison ya kuwapiga chenga walinzi wa Gendarmerie na kutoa pasi iliyozaa bao.

Mugalu alitupatia bao la tatu dakika ya 78 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Kibu Denis kufuatia shambulizi lililoanzia kwa Jonas Mkude na Shomari Kapombe.

Mlinda mlango wa Gendarmerie Saidou Hamishe alijifunga na kutupatia bao la nne dakika ya 84 baada ya kurudishiwa mpira na mlinzi wake ambao ulionekana hauna madhara.

Kocha Pablo Franco aliwatoa Pape Sakho, Morrison, Rally Bwalya na Mugalu kuwaingiza Kibu, Taddeo Lwanga, Peter Banda na Medie Kagere.

Ushindi huu umetufanya kufikisha pointi 10 tukimaliza nafasi ya pili nyuma ya RS Berkane ambao tupo nao sawa kwa alama na uwiano wa mabao lakini wakiwa juu kutokana na goli moja zaidi walilotufunga katika mechi mbili tulipokutana.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER