Tumetimba mguu mmoja ndani Makundi Afrika

Ushindi mnono wa mabao 3-1 tuliopata kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Premiero De Agosto uliopigwa Uwanja wa Novemba 11 nchini Angola umetufanya kuingiza mguu mmoja katika hatua ya makundi.

Katika mchezo huo, Clatous Chama alitupatia bao la kwanza dakika ya nane baada ya kumpiga chenga mlinzi mmoja wa De Agosto na kupiga shuti kali la chini chini akimalizia krosi iliyopigwa na Augustine Okrah.

Baada ya bao hilo tuliendelea kulishambuliana kwa zamu ambapo dakika ya 42 alimanusura Chama atupatie bao la pili kufuatia krosi iliyopigwa na Israel Patrick kumgonga mguuni.

Kipindi cha pili wenyeji De Agosto walirudi kwa kasi ambapo dakika 10 za mwanzo waliliandama lango letu ingawa tulisimama imara kuhakikisha tunakuwa salama.

Mlinzi wa kulia Israel Patrick alitupatia bao la pili dakika ya 62 kwa shuti kali ndani ya 18 akimalizia pasi ya Sadio Kanoute kufuatia shambulizi lililoanzishwa na Mzamiru Yassin.

Moses Phiri alitupatia bao la tatu dakika ya 75 baada ya kumalizia pasi safi ya Chama ambalo halikudumu kufuatia De Agosto kufunga muda huo huo kwa mkwaju wa penati lililofungwa Tshibamba Dago.

Kocha Juma Mgunda alifanya mabadiliko ya kuwatoa Okrah, Kibu Denis na Phiri na kuwaingiza Kennedy Juma, John Bocco na Pape Sakho.

Ushindi huu umetuweka kwenye mazingira mazuri ambapo katika mchezo wetu wa marudiano utakaopigwa wiki ijayo jijini Dar es Salaam tutahitaji ushindi wowote au sare ili kutinga hatua ya makundi.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER