Mchezo wetu wa kwanza wa kirafiki dhidi ya Turan Tovuz PFK ya Azerbaijan uliofanyika katika Uwanja wa Soğuksu Spor Kompleksi umemalizika kwa ushindi wa mabao 2-0.
Mchezo huo ambao umechezwa dakika 60 ulikuwa mzuri kwa timu zote kushambuliana kwa zamu lakini dakika 30 hakuna bao lililopatikana.
Kipindi cha pili Kocha Mkuu Roberto Oliviera ‘Robertinho’ alifanya mabadiliko ya kuwaingiza Kibu Denis na John Bocco kuchukua nafasi za Shaban Chilunda na Moses Phiri na kuongeza kasi katika safu ya ushambuliaji.
Dakika ya 44 Kibu alitupatia bao la kwanza baada ya mlinzi wa Turan, Eltun Turabov kufanya makosa katika jitihada za kuokoa.
Nahodha John Bocco alikamilisha ushindi kwa kufunga la pili dakika ya 56 baada ya kupokea pasi safi ya Jean Baleke.
Saa 12 jioni tutacheza mechi ya pili dhidi ya Turan ambayo tutawapa nafasi wachezaji wengine ambao hawajacheza kwenye mchezo wa kwanza.