Kikosi chetu leo kimefanikiwa kupata ushindi mnono wa mabao 6-0 katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Abo Hamad inayoshiriki ligi daraja la pili nchini Misri.
Mchezo ulianza kwa kasi huku timu zote zikishambuliana lakini sisi tulimiliki sehemu kubwa huku Jonas Mkude na Victor Akpan wakifanya vizuri katikati ya uwanja.
Moses Phiri alitupatia bao la kwanza dakika ya 44 baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Clatous Chama.
Mkude alitupatia bao la pili dakika ya 58 akimalizia pasi ya Augustine Okrah kabla ya Medie Kagere aliyetokea benchi kuongeza la tatu dakika ya 69 baada ya kupokea pasi ya Peter Banda.
Pape Sakho ambaye naye alitokea benchi alitufungia bao la nne na la tano dakika za 71 na 86 huku akionyesha kiwango bora sambamba na Banda.
Erasto Nyoni alikamilisha karamu ya mabao kwa kufunga bao mwisho dakika ya 90 na kuufanya usiku wa Wanasimba kuwa wa furaha.
Kocha Zoran Maki aliwatoa Gadiel Michael, Mkude, Israel Patrick, Okrah, Phiri, Akpan, Henok Inonga, Clatous Chama Habib Kyombo na kuwaingiza, Nyoni, Jimmyson Mwanuke, Mohamed Ouattara, Banda, Chris Mugalu, Taddeo Lwanga, Nassor Kapama, Sakho, na Kagere.
Mchezo wa leo ni wa pili wa kirafiki baada ya ule wa kwanza uliofanyika wiki moja uliopita dhidi ya Ismailia na kumalizika kwa sare ya bao moja.