Kikosi chetu kimepata sare ugenini ya mabao 2-2 dhidi ya Power Dynamos katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliofanyika katika Uwanja wa Levy Mwanawasa, Ndola Zambia.
Tulianza mchezo taratibu huku tukiwasoma wapinzani Power Dynamos ambao wakitawala sehemu kubwa.
Mlinda mlango Ayoub Lakred aliokoa mashambulizi mawili ya hatari dakika za 16 na 22 ambayo yangeweza kututoa mchezoni.
Wenyeji Power Dynamos walipata bao la kwanza dakika ya 27 kupitia kwa Joshua Mutale baada ya kuwazidi ujanja walinzi wetu.
Dakika 58 Clatous Chama alitufungia bao la kusawazisha kufutia shuti kali lililopigwa na Mzamiru Yassin kuokolewa na mlinda mlango wa Power Dynamos.
Caphers Mulombwa aliipatia Power Dynamos bao la pili dakika ya 74 kwa shuti kali nje ya 18 lililomchanganya mlinda mlango Ayoub Lakred.
Mshambuliaji, Jean Baleke alipoteza nafasi tatu za wazi za kufunga ambazo kama angezitumia vizuri tungerejea nyumbani na ushindi mnono.
Mlinzi wa kati wa Power Dynamos, Dominick Chanda alitolewa kwa kuonyeshwa kadi nyekundu dakika ya 84 baada ya kumchezea madhambi Jean Beleke.
Chama alitupatia bao la kusawazisha dakika ya nne ya yanyongeza kipindi cha pili kwa shuti kali la mguu wa kushoto akiwa nje ya 18.
X1: Lakred, Kapombe, Zimbwe Jr (Bocco 90+1) Che Malone, Henock, Kanoute (Ngoma 45’), Kibu (Miquissone 79’) Mzamiru, Phiri (Baleke 45’) Chama, Onana (Ntibazonkiza 61’)