Tumejipanga kumaliza kazi leo kwa Mkapa

Kikosi chetu leo kitashuka katika Uwanja wa Benjamin Mkapa saa moja usiku kuikabili Orlando Pirates ya Afrika Kusini kwenye mchezo wa kwanza wa Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Dhamira yetu ni kuhakikisha tunautumia vizuri uwanja wa nyumbani kupata ushindi mnono ili tukienda Afrika Kusini kwenye mchezo wa marudiano tuwe na mtaji mkubwa wa mabao.

Imepita miaka 29 tangu tulipoingia fainali ya michuano hii ambayo ilikuwa ikijulikana kama Kombe la CAF na safari hii tunataka kuifikia rekodi yetu na ikiwezekana kuivunja.

HII HAPA MIPANGO YA PABLO

Kocha Mkuu Pablo Franco, ameweka wazi kuwa kikosi kipo tayari kwa ajili ya mchezo na matumaini ya kuibuka na ushindi ni makubwa kutokana na maandalizi tuliyofanya.

Pablo amesema katika mchezo wa leo hatuhitaji alama tatu bali tunahitaji kufuzu kwenda nusu fainali kwa hiyo tunapaswa kushinda nyumbani kwa idadi kubwa ya mabao.

Katika mchezo wa leo Pablo amesema tutakuwa na faida ya hali ya uwanja (atmosphere) kutokana na kuruhusiwa kuujaza hivyo anaamini mashabiki watajitokeza kwa wingi kutupa sapoti.

“Katika mchezo wa leo hatuhitaji alama tatu bali tunatakiwa kufuzu kwa hiyo ili kufanikisha hilo tunapaswa kupata ushindi mnono nyumbani ili tukienda kwao tusiwe na presha,” amesema Pablo.

WACHEZAJI WANAPENDA MECHI KUBWA

Mlinzi wa kulia Shomari Kapombe, amesema wao kama wachezaji walifurahi tulivyopangwa na Orlando kwa kuwa wanapenda kucheza mechi kubwa ambazo zinavutia mashabiki.

“Tulivyoingia robo fainali tulikuwa tayari kucheza na timu yoyote lakini tulivyopangwa na Orlando tulifurahi sababu tunapenda kucheza mechi kubwa. Tupo tayari kwa mchezo, tumefanya mazoezi kwa wiki nzima kila kitu kipo sawa,” amesema Kapombe.

HISTORIA KUANDIKWA

Mchezo wa leo utakuwa wa kwanza katika historia ya soka nchini kutokana na kutumika Teknolojia ya Usaidizi wa Video kwa Waamuzi (VAR).

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER