Tumejipanga kumaliza kazi kwa Mkapa leo

Kikosi chetu leo saa 10 jioni kitashuka katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili Premiero De Agosto katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Tunaingia katika mchezo wa leo tukiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa mabao 3-1 tuliopata katika mchezo wa mzunguko wa kwanza nchini Angola.

Ushindi huo bado hautupi uhakika wa kujihakikisha kufuzu moja kwa moja badala yake tumejipanga kupambana kuanzia dakika ya kwanza ili kuwapa furaha mashabiki wetu.

MGUNDA: TUPO TAYARI KWA MCHEZO

Akizungumzia mchezo huo, Kocha Mkuu Juma Mgunda, amesema maandalizi yamekamilika kwa asilimia 100 na wachezaji wapo kwenye hali nzuri na morali ipo juu tayari kuhakikisha wanapeperusha vema bendera ya taifa.

Mgunda ameongeza kuwa tunakutana na timu ambayo tumeiona na tunaijua hivyo tumejiandaa kuhakikisha tunatumia vizuri mapungufu yao kupata ushindi nyumbani kuwapa furaha mashabiki wetu.

“Naweza kusema maandalizi yamekamilika kwa asilimia 100, wachezaji wote wapo kwenye hali nzuri kuhakikisha wanatetea bendera ya taifa na kuwapa furaha Wanasimba,” amesema Mgunda.

MZAMIRU AFUNGUKA

Kiungo mkabaji Mzamiru Yassin amesema wachezaji wote wanajua umuhimu wa mchezo huo pamoja na malengo ya klabu kwenye michuano hiyo hivyo watahakikisha wanafanikisha.

Mzamiru amesema De Agosto sio timu nyepesi kama wengi wanavyodhani kwakuwa tumewafunga kwao na haitakuwa mechi rahisi kwetu lakini tumejipanga kuhakikisha tunashinda.

“Malengo yetu kama klabu kwanza nikufuzu hatua ya makundi, ni kweli tumepata ushindi mzuri ugenini lakini tunajua mchezo utakuwa mgumu lakini tumejipanga.

“Tumepata maandalizi mazuri kutoka kwa walimu wetu na sisi wachezaji tupo tayari kuhakikisha tunafanya tunaloweza kuwapa furaha Wanasimba,” amesema Mzamiru.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER