Kikosi chetu kimefanikiwa kuondoka na alama zote tatu baada ya kuichakaza Ruvu Shooting mabao 4-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Katika mchezo huo, kiungo Jonas Mkude alishindwa kuendelea na mchezo na kutolewa dakika ya 23 baada ya kuumizwa mguu na Haruna Chanongo nafasi yake ikachukuliwa na Rally Bwalya.
Kibu Denis alitupatia bao la kwanza dakika ya 39 kwa shuti kali la mguu wa kushoto baada ya krosi ya Shomari Kapombe kuunganishwa na Peter Banda kabla ya mlinzi wa Ruvu kuondoa mpira uliomkuta mfungaji.
Bwalya alitupatia bao la pili kwa shuti kali la mguu wa kushoto nje ya 18 dakika ya 66 baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Pape Sakho.
Nahodha John Bocco alitupatia bao la tatu kwa shuti kali ndani ya 18 dakika ya 81 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Yusuf Mhilu.
Dakika moja baadaye Ruvu walipata bao la kufutia machozi kupitia kwa Chanongo baada ya kupokea pasi kutoka Abrahman Musa.
Mlinzi wa kati Henock Inonga alitupatia bao la nne kwa kichwa dakika ya 84 akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na Israel Patrick.
Kocha Pablo Franco aliwatoa Mkude, Medie Kagere, Peter Banda, Mzamiru Yassin, Kapombe na kuwaingiza Bwalya, Bocco, Mhilu, Israel Patrick na Kennedy Juma.