Tuko tayari kwa Dodoma Jiji leo

Kikosi chetu leo saa moja usiku kitashuka katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili Dodoma Jiji katika muendelezo wa Ligi Kuu ya NBC 2021/22.

Mchezo wa leo utakuwa wa pili wa mzunguko wa pili wa ligi baada ya ule wa kwanza dhidi ya Biashara United tuliocheza Ijumaa na kuibuka na ushindi wa mabao 3-0.

Ligi ipo mzunguko wa pili na kila timu kwa sasa inahitaji ushindi ili kujiweka mahali pazuri na tunajua mchezo wa leo utakuwa mgumu na Dodoma watatupa upinzani mkubwa.

KAULI YA KOCHA PABLO

Kocha Mkuu Pablo Franco, ameweka wazi kuwa mchezo utakuwa mgumu na tutaingia kwa tahadhari zote ili kukamilisha malengo ya kuchukua alama tatu yanatimia.

Amesema ingawa ratiba imekuwa ngumu hatupati muda wa kujiandaa kutoka mechi moja hadi nyingine lakini tutapambana kuhakikisha tunafanya jitihada na kubakisha pointi tatu nyumbani.

Raia huyo wa Hispania amesema wachezaji watakaokuwa tayari kimwili na kiakili kuelekea mchezo wa leo atawapa nafasi kwa sababu wanachoka sana kutokana na ugumu wa ratiba.

“Ratiba ni ngumu, uwiano wa mechi moja na nyingine ni mdogo, hatuna muda wa kutosha kujiandaa na kufanya mazoezi ya utimamu wa mwili. Ndiyo maana tunakuwa na majeruhi wengi kikosini.

“Tunafahamu mchezo utakuwa mgumu, Dodoma ni timu nzuri lakini tumejipanga kuhakikisha tunawakabili na kuchukua pointi zote tatu,” amesema Pablo.

HALI YA KIKOSI

Wachezaji wako katika hali nzuri, morali ipo juu na kila mmoja anatamani kuaminiwa na benchi la ufundi ili atuwakilishe. Nyota wetu waliokuwa majeruhi hali zao zinaendelea kuimarika na wengi wameanza mazoezi pamoja na wenzao.

MARA YA MWISHO TULIVYOKUTANA

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma Oktoba Mosi mwaka jana tuliibuka na ushindi wa bao moja lililofungwa na Medie Kagere dakika ya 68 akimalizia pasi ya kichwa iliyopigwa na Chris Mugalu.

SHARE :
Facebook
Twitter

2 Responses

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER