Tuko tayari kuchukua pointi tatu kwa Polisi leo

Kikosi chetu leo saa 10 jioni kitashuka katika Uwanja wa Ushirika Moshi mkoani Kilimanjaro kuikabili Polisi Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC.

Ligi inaelekea ukingoni na kila timu inajidhatiti kuhakisha inashinda lakini sisi kama mabingwa watetezi tumejipanga kukusanya alama tatu katika mchezo huo.

Dhamira yetu ni kuhakikisha tunakusanya alama kwenye kila mchezo wa mzunguko wa pili wa ligi ili kutetea ubingwa wetu.

PABLO ALIA NA UGUMU WA RATIBA

Kocha Mkuu Pablo Franco amesema licha ya ugumu wa ratiba yetu ambayo inatufanya kukosa muda wa kutosha kujiandaa kutoka mechi moja hadi nyingine lakini tutapambana kupata alama tatu.

Pablo amesema mchezo utakuwa mgumu kwa kuwa hatujapata muda mzuri wa kufanya mazoezi pia tunakwenda kucheza katika uwanja ambao sehemu ya kuchezea siyo rafiki.

“Mchezo utakuwa mgumu zaidi kwetu, hatujapata muda wa kufanya mazoezi. Tumesafiri juzi kwa basi kuja hapa tukitoka Tanga jana wachezaji wamefanya mazoezi na leo mechi, kwa hiyo hatujapumzika. Lakini tutapambana,” amesema Pablo.

KAPOMBE AITAJA ORLANDO PIRATES

Mlinzi wa kulia, Shomari Kapombe amesema ushindi katika mchezo wa leo utaongeza hamasa kuelekea mechi yetu ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Orlando Pirates.

Kapombe amesema tutajitahidi kupata alama tatu ili wikiendi ijayo tukikutana na Orlando tuwe katika hali nzuri.

“Tunahitaji sana ushindi kwenye mchezo wa leo. Ushindi utaongeza hamasa kwetu wachezaji, benchi la ufundi na mashabiki kuelekea mchezo wetu wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Orlando,” amesema Kapombe.

HALI YA KIKOSI

Jambo jema ni kwamba wachezaji wote waliosafiri wapo kwenye hali nzuri morali ipo juu na hakuna aliyeumia katika mchezo wetu uliopita au mazoezini wote wapo tayari kwa mechi.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER