Tuko kamili kwa ajili ya mtani leo

Kikosi chetu leo kitashuka katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuwakabili watani wetu wa jadi Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC ambao utaanza saa 11 jioni.

Tunaingia kwenye mchezo wa leo tukiwa tunajua haitakuwa rahisi kwa kuwa mara zote derby inakuwa ngumu lakini tuko tayari kuhakikisha tunapambana mpaka mwisho.

Mbali na alama tatu ambazo tunazihitaji lakini ushindi kwenye mchezo wa leo utawafanya Wanasimba kuwa na furaha kitu ambacho tutapambana ili kukitimiza.

MGUNDA AFUNGUKA

Kocha Mkuu Juma Mgunda, amesema maandalizi ya mchezo yamekamilika na wachezaji wapo kwenye hali nzuri tayari kwa mtanange huo ambao unasubiriwa kwa hamu na wadau wa soka ndani na nje ya nchi.

Mgunda amesema utakuwa mchezo mgumu wa ushindani lakini tumejipanga vizuri kuhakikisha tunashinda na kuchukua alama tatu muhimu.

“Mchezo utakuwa mgumu, lakini sisi tumejiandaa kuhakikisha tunashinda na kupata alama tatu huku tukicheza aina yetu ya mpira tuliyoizoea. Mechi ya Derby ni ngumu lakini tupo tayari,” amesema Mgunda.

ZIMBWE JR ATOA AHADI KWA MASHABIKI

Nahodha Msaidizi, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ amewaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi huku akisema watahakikisha wanapambana kushinda ili kuwapa furaha.

Zimbwe Jr amesema wachezaji wote wanajua umuhimu wa mchezo na jinsi Wanasimba wanavyouchukulia hivyo wamejipanga kuhakikisha wanawapa furaha.

“Kwa upande wetu wachezaji tupo tayari kwa mchezo, tunahitaji alama tatu kwa ajili ya kujiimarisha kileleni pia tuwapa furaha mashabiki wetu,” amesema Zimbwe Jr.

KAPOMBE, MWANUKE KUIKOSA DERBY

Katika mchezo huo, Kocha Mgunda amethibitisha wachezaji wawili Shomari Kapombe na Jimmyson Mwanuke ndio pekee ambao hawatakuwa sehemu ya mchezo kutokana na kuendelea kuuguza majeraha.

Kapombe amerejea mazoezini lakini bado hayupo timamu asilimia 100 hivyo hatakuwa sehemu ya mchezo kama ilivyo kwa Mwanuke.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER