Kikosi chetu kimefanya mazoezi ya mwisho katika Uwanja wa New Amaan Complex tayari kwa mchezo wa kesho wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Azam FC utakaopigwa saa 2:30 usiku.
Mazoezi hayo yameanza saa mbili usiku muda ule ule ambao mchezo wetu wa kesho utapigwa.
Kikosi kiliwasili hapa Zanzibar leo mchana ambapo kilielekea Ikulu ya Zanzibar baada ya kupokea mwaliko kutoka kwa Rais Dkt. Hussein Ally Mwinyi.
Kocha Mkuu Fadlu Davids ameweka wazi mbele ya Waandishi wa Habari kuwa utakuwa mchezo mgumu kutokana na ubora wa Azam lakini hata hivyo tupo tayari kwa ajili ya kupambana na kupata pointi tatu.
“Azam imebadilika kiuchezaji tangu alipokuja kocha mpya, nimewatazama kwenye mechi tatu zilizopita wako vizuri lakini nasi tumejiandaa kuwakabili,” amesema Kocha Fadlu.
Katika mazoezi hayo ambayo yameongozwa na Kocha Fadlu na wasaidizi wake hakuna mchezaji aliyepata maumivu ambayo yatamfanya kuukosa mchezo wa kesho.