Kikosi chetu kimefanya mazoezi katika Uwanja wa Cairo International usiku huu uwanja ambao tutautumia katika mchezo wetu wa marudiano wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly utakaopigwa keshokutwa Ijumaa.
Kanuni za CAF zinataka timu mgeni kufanya mazoezi katika Uwanja utakaotumika siku moja kabla ya mchezo lakini kutokana na kesho dimba hilo litakuwa na matumizi mengine hivyo tumetakiwa kufanya mazoezi leo.
Wachezaji wote 23 ambao tumesafiri nao kwa ajili ya mchezo huo wameshiriki mazoezi hayo na hakuna yoyote ambaye amepata maumivu ambayo yanaweza kumfanya kuukosa mchezo wa Ijumaa.
Pamoja na kujua tuna kibarua kigumu kucheza na timu bora ugenini tukiwa nyuma kwa bao moja lakini wachezaji wana morali kubwa na matumaini ya kufuzu hatua ya nusu fainali ni makubwa.