Timu Kuingia Kambini jioni Kujiandaa na Horoya

Kikosi chetu kitaingia kambini baada ya mazoezi ya jioni kujiandaa na mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Horoya kutoka Guinea utakaopigwa Jumamosi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa saa moja usiku.

Baada ya ushindi wa mabao 3-0 tuliopata dhidi ya Mtibwa Sugar siku ya Jumamosi katika Uwanja wa Manungu Complex wachezaji walipewa mapumziko ya siku moja na leo wanaingia kambini.

Meneja Habari na Mawalisiano wa klabu, Ahmed Ally amesema kiungo mshambuliaji Kibu Denis amepona majeraha yaliyokuwa yanamsumbua na ataungana na wenzake katika mazoezi ya leo jioni.

Kibu alipata majeraha katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa ugenini dhidi ya Vipers uliopigwa nchini Uganda Februari 25, ambapo kwa sasa yupo fiti na anategemewa kuwa sehemu ya kikosi kitakachoshuka dimbani kuikabili Horoya.

Ahmed amesema kiungo mkabaji, Ismael Sawadogo aliyekuwa anasumbuliwa na maumivu ya nyonga nae ataingia kambini pamoja na wenzake lakini atafanyiwa vipimo kwanza ili kujua maendeleo yake.

“Kikosi kitaingia kambini baada ya mazoezi na jambo jema wachezaji wetu waliokuwa majeruhi Kibu na Sawadogo nao watakuwa sehemu ya kikosi.

“Mchezaji pekee ambaye tutamkosa ni Augustine Okrah ambaye nae ameanza mazoezi ya pekee yake kutokana na jeraha lake kuendelea vizuri,” amesema Ahmed.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER