Timu imefanya mazoezi ya mwisho tayari kuivaa Mtibwa

Kikosi chetu kimefanya mazoezi ya mwisho leo jioni katika Uwanja wa Highland tayari kwa mchezo wa kesho wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Mtibwa Sugar.

Wachezaji wote waliosafiri wamefanya mazoezi na hakuna aliyepata majeraha hivyo benchi la ufundi litakuwa na wigo mpana wa kuchagua kikosi.

Kocha Mkuu Pablo Franco, amesema licha ya Uwanja wa Manungu ambao tutautumia katika huo kutokuwa rafiki sana kwa aina ya soka tunalocheza lakini tumejipanga kutandaza kandanda safi.

Pablo ameongeza kuwa baada ya kushindwa kupata matokeo katika mchezo uliopita tumejiandaa kuhakikisha tunashinda ili kurejesha hali ya kujiamini kikosini.

“Tumefanya mazoezi ya mwisho kabla ya mchezo wa kesho, wachezaji waki katika hali nzuri. Tunataraji kucheza soka safi ingawa tunajua uwanja hautakuwa rafiki kwetu,” amesema Pablo.

Kwa upande wake, mlinda mlango Aishi Manula amesema mchezo utakuwa mgumu na siku zote timu ndogo ikikutana na kubwa inajipanga vizuri lakini pamoja na hayo kesho itakuwa zamu yetu kufurahi.

“Mtibwa ni timu nzuri na mara zote wakikutana nasi mechi inakuwa ngumu lakini tupo tayari kuwakabili. Tunawaomba mashabiki zetu wajitokeze kwa wingi kuja kutusapoti naamini hatutawaangusha,” amesema Manula.

SHARE :
Facebook
Twitter

One Response

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER