Kampuni ya Michezo ya kubahatisha ya SportPesa ambao ni wadhamini wetu wakuu, imeitukabidhi hundi ya Sh milioni 100 kama bonasi baada ya kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Msimu wa 2020/21.
Tukio hilo la makabidhiano limefanyika katika Ofisi za SportPesa zilizopo Masaki jijini Dar es Salaam ambapo kiasi hicho cha fedha ni sehemu ya makubaliano ya mkataba tulioingia nao na kwa miaka minne mfululizo tumeendelea kuichukua.
Mkurugenzi wa Uendeshaji wa SportPesa, Tarimba Abbas ametupongeza kwa mafanikio tuliyopata msimu huu na ameweka wazi kuwa wana furaha kwa sababu tumeendelea kuitangaza vizuri SportPesa.
Tarimba amesema mkataba wetu umebaki mwaka mmoja na wapo tayari kukaa chini kufanya mazungumzo kwa ajili ya kuongeza mkataba ambao utakuwa na maslahi zaidi kuliko unaoisha.
“Leo tumeikabidhi Simba hundi ya Sh milioni 100 kama bonasi kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2020/21 ikiwa ni sehemu ya mkataba.
“Kipekee naipongeza Simba kwa kuendelea kuitangaza vizuri SportPesa na tunajivunia kwa hilo,” amesema Tarimba.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa klabu, Barbara Gonzalez ameipongeza SportPesa kwa kufuata kila makubaliano yaliyopo kwenye mkataba na kuwaahidi kuendelea kuitangaza kwa kufanya vizuri ndani na nje ya nchi.
“Naipongeza SportPesa kwa kufuata kila makubaliano yaliyopo kwenye mkataba kwa kutoa bonus na hii inatufanya kutaka kuendelea kufanya nao kazi na tupo kwenye mazungumzo ya kusaini mkataba mpya,” amesema Barbara.
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji, mlinzi wa kushoto, Gadiel Michael ameipongeza SportPesa kwa kuendelea kufuata makubaliano ya mkataba na wapo tayari kuendelea kufanya vizuri uwanjani ili kuitangaza.