Simba yalipa kisasi yawapigisha kwata Ruvu Shooting Kirumba

Hatimaye timu yetu leo imefanikiwa kulipa kisasi kwa Ruvu Shooting kwa kuwatandika mabao 3- katika mchezo wa ligi kuu uliopigwa katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Mchezo huu ni wa kisasi sababu Ruvu walitufunga bao moja kwenye mechi ya mzunguko wa kwanza uliopigwa katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, Novemba mwaka jana.

Nahodha John Bocco alitufungia bao la kwanza dakika ya 17 baada ya kumalizia mpira wa krosi uliopigwa na Luis Miquissone.

Chris Mugalu alitupatia bao la pili dakika ya 61 baada ya kumalizia mpira wa krosi uliopigwa na Bernard Morrison.

Ruvu walimaliza mpira wakiwa pungufu baada ya Nahodha wao Juma Nyoso kuonyeshwa kadi nyekundu dakika ya 72 baada ya kumpiga makusudi kisogoni Shomari Kapombe kabla ya mlinda mlango Abdallah Rashid naye kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 85.

Dakika ya 87 Bocco alitufungia bao la tatu kwa mkwaju wa penati baada ya Morrison kufanyiwa madhambi ndani ya 18 na mlinda mlango Abdallah Rashid yaliyomfanya kuonyeshwa kadi nyekundu.

Kocha Didier Gomes aliwapumzisha Mugalu, Hassan Dilunga na Rally Bwalya na kuwaingiza Morrison, Mzamiru Yassin na Saidi Ndemla.

Matokeo haya yametufanya kufikisha pointi 67 baada ya kucheza mechi 27 tukiwa na michezo miwili mkononi.

SHARE :
Facebook
Twitter

2 Responses

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER