Simba yabakisha tatu kutwaa ubingwa VPL

Ushindi wa mabao 4-1 tuliopata dhidi ya Mbeya City leo umetufanya tubakishe alama tatu ili kuwa  mabingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Msimu wa 2020/21.

Endapo tutaibuka na ushindi katika mchezo ujao tutafikisha pointi 76 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote hivyo tutakuwa mabingwa.

Katika mchezo wa leo, Rally Bwalya alitupatia bao la kwanza dakika ya 31 kwa shuti kali ndani ya 18 kufuatia mpira wa kwanza kuzuiwa na walinzi wa City kabla ya kumkuta tena na kupiga moja kwa moja wavuni.

Dakika nne baadaye, Luis Miquissone alitufungia bao la pili kwa shuti kali ndani ya 18 baada ya mpira wa kwanza kugonga mwamba na kumkuta tena kisha kupiga la chini chini lililomshinda mlinda mlango Haroun Mandanda.

Nahodha John Bocco alitufungia bao la tatu dakika ya 48 baada ya kumalizia mpira wa krosi uliopigwa na Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’.

Pastory Athanas aliifungia City bao la kwanza dakika ya 52 baada ya kumalizia kazi nzuri iliyofanywa na George Sangija.

Clatous Chama alitupatia bao la nne dakika ya 83 baada ya kumalizia kazi nzuri iliyofanywa na Shomari Kapombe.

Kocha Didier Gomes aliwatoa Bwalya, Bocco na Bernard Morrison na kuwaingiza Clatous Chama, Medie Kagere na Mzamiru Yassin.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER