Baada ya mapumziko ya wiki mbili kupisha mechi za kimataifa za Timu ya Taifa, kikosi chetu leo kinarejea katika Uwanja wa CCM Kirumba kuikabili Polisi Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Tunaingia kwenye mchezo huo tukizitaka pointi tatu nyingine kutoka kwa maafande hao wa polisi kama tulivyozichukua Desemba 9, mwaka jana kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa kuwafunga mabao 2-0 ambayo yote yalifungwa na Clatous Chama.
Katika kipindi hiki kuelekea ukingoni mwa ligi kuu tunahitaji kushinda michezo yote ili kutetea ubingwa wetu kwa mara ya nne mfululizo.
Kuelekea mchezo wa leo Kocha Msaidizi, Seleman Matola amesema wachezaji wote wapo kwenye hali nzuri na tayari kupambana kwa ajili ya kuhakikisha pointi tatu zinapatikana.
“Licha ya kuwafunga katika michezo mitatu ya ligi iliyopita lakini haimaanishi kama mechi ya leo itakuwa rahisi hivyo tutahakikisha tunaongeza juhudi ili kupata alama tatu.
“Kikosi kipo kamili wachezaji wote wapo kwenye hali nzuri, tunawaheshimu Polisi mara zote tukikutana wanatupa ushindani mkubwa lakini tumejipanga kuhakikisha tunashinda,” amesema Matola.
Kwa upande wake Nahodha Msaidizi, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ amesema morali za wachezaji zipo juu na jambo pekee lililo vichwani mwao ni kuhakikisha tunashinda kila mchezo ili kutetea ubingwa.
TAARIFA YA KIKOSI
Katika mchezo wa leo tutawakosa nyota wetu Clatous Chama ambaye ana matatizo ya kifamilia na Jonas Mkude ambaye suala lake la kinidhamu bado halijamalizika.
3 Responses
Mechi muhimu na Ngumu Leo,naamini hatutafanya makosa ya kuwapa hata goli Polisi,kila la heri Wanajeshi wetu
tatizo hamuekagi line up sjui kwa nini ila tunajivunia timu yetu
Kila la kheri timu yetu Pendwa.
Ushindi ni mhimu.