Simba, Mtibwa ni mechi ya kumaliza ubishi

Baada ya kumaliza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, leo tunarejea kwenye Ligi Kuu ya Vodacom ambapo tutashuka dimbani kuikabili Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Mchezo wa leo utakuwa ni wa kumaliza ubishi kutokana na mechi ya mzunguko wa kwanza uliopigwa Septemba 12 mwaka jana katika Uwanja wa Jamhuri Morogoro kumalizika kwa sare ya bao moja.

Kikosi chetu kinaingia kwenye mchezo wa leo kikiwa na morali ya hali juu kutokana na kumaliza hatua ya makundi ya Ligi ya mabingwa Afrika tukiwa vinara wa kundi A kwa kufikisha alama 13.

TAARIFA ZA VIKOSI

Kocha Msaidizi, Selemani Matola amesema hakuna mchezaji ambaye atakosekana kutokana na kuwa majeruhi au sababu yoyote wote wako kambini na morali ipo juu kuelekea mchezo wa leo.

Matola amekiri mchezo utakuwa mgumu kutokana na ukweli kwamba mara kadhaa tunapokutana na Mtibwa mechi inakuwa ngumu akitolea mfano kipindi hiki ambapo hawako kwenye nafasi nzuri kwenye msimamo kuwa sababu inayoongeza ugumu.

“Mtibwa ni timu ngumu na mara zote tukikutana mechi inakuwa ngumu lakini sisi tumejiandaa kuwakabili, wachezaji wote wapo kambini na wamefanya mazoezi hakuna tutakayemkosa,” amesema Matola.

ZIMBWE ATOA NENO

Nahodha Msaidizi, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ amewataka mashabiki wetu kujitokeza kwa wingi uwanjani kuwapa hamasa kwani wanaruhusiwa kuja idadi yoyote hawazuiwi kama ilivyokuwa katika mechi za Ligi ya Mabingwa.

“Leo mashabiki wanaruhusiwa kuingia uwanjani kwa idadi yoyote kwa hiyo nawaomba Wanasimba wajitokeze kwa wingi ili kuiona timu yao na tunaamini tutapata ushindi,” amesema Zimbwe.

SHARE :
Facebook
Twitter

One Response

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER