Simba kushusha kikosi Kamili dhidi ya Namungo Kesho

Kuelekea kukamilisha msimu wa Ligi Kuu 2020/21, benchi la ufundi limeweka wazi kesho tutashusha kikosi kamili katika mchezo dhidi ya Namungo FC ambao tutakabidhiwa taji letu la ubingwa.

Katika mechi mbili zilizopita tulitumia baadhi ya wachezaji ambao hawakupata nafasi nyingi za kucheza msimu huu lakini kesho kwakua ni siku ya sherehe na tunahitaji ushindi tutapanga kikosi kamili.

Kocha Msaidizi Seleman Matola amesema inapendeza kukabidhiwa ubingwa baada ya kupata ushindi na ndiyo maana tutapanga kikosi kamili ambacho kimetumika msimu mzima.

Matola amesema katika misimu miwili iliyopita tulikabidhiwa ubingwa lakini tumepoteza na kutoka sare lakini kwa kesho tumejipanga kuhakikisha tunapata ushindi ili kunogesha sherehe.

“Kwanza tuna bahati na Namungo, msimu uliopita tulikabidhiwa kombe mbele yao lakini tulitoka sare kesho tunaenda kukabidhiwa tena dhidi yao lakini haitakuwa kwa sare bali ushindi,” amesema Matola.

Matola amewataka mashabiki wetu kujitokeza kwa wingi uwanjani sababu ndio mchezo wa mwisho wa ligi na pia unatumika kukabidhiwa ubingwa.

“Mashabiki wetu wamekuwa nasi kwa msimu mzima, kesho ni siku ya mwisho na sherehe ya ubingwa hivyo itapendeza kama watajitokeza kwa wingi. Sisi tunawaahidi ushindi ili kusindikiza sherehe za ubingwa,” amesema Matola.

SHARE :
Facebook
Twitter

One Response

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER