Simba kujipima tena leo nchini Morocco

Kikosi chetu leo jioni kitacheza mchezo wa pili wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Olimpique Club De Khouribga ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea msimu mpya wa ligi 2021/22 hapa nchini Morocco.

Katika mchezo wa leo tutawatumia zaidi wachezaji wapya tuliowasajili kutokana na nyota wetu 12 kuruhusiwa kujiunga na timu zao za Taifa huku watatu wakitolewa kwa mkopo na mlinda mlango Beno Kakolanya akirudi nchini kushiriki mazishi ya mama yake mzazi.

Mchezo wa leo utakuwa ni wa pili baada ya ule wa kwanza tuliocheza Agosti 21 na FAR Rabat na kutoka sare ya mabao mawili.

Kocha Mkuu Didier Gomes amesema anafurahishwa na jinsi wachezaji wanavyoelewa mafunzo wanayowapa kwa haraka kitu anachoamini litakuwa jambo zuri kuelekea msimu mpya.

Gomes amewasifu pia wachezaji wapya tuliowasajili kutokana na kuzoea haraka mazingira ya kikosi chetu pamoja na wachezaji wenzao kitu ambacho kinamrahisishia kazi mazoezini.

“Leo tunacheza mechi ya pili ya kirafiki dhidi ya Khouribga na tutatumia zaidi wachezaji wapya tuliowasajili kutokana na wengine 12 kwenda kujiunga na timu za taifa.

“Maandalizi yanaendelea vizuri na nafikiri baada ya siku tano mpaka wiki muunganiko wa kikosi utakuwa vizuri zaidi na ninaamini tutaendelea kufanya vizuri msimu ujao,” amesema Gomes.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER