Kuelekea mchezo wa kesho wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Kocha Msaidizi Selemani Matola amesema kikosi kipo kamili hakuna mchezaji atakayekosekana kutokana na kuwa majeruhi au sababu nyingine.
Matola amesema wachezaji wote wapo kambini na wamefanya mazoezi hivyo watakuwa na wigo mpana wa kuchagua kikosi kitakachoshuka dimbani kuikabili Mtibwa kesho.
Amesema anafahamu mchezo utakuwa mgumu na amekiri Mtibwa ni moja ya timu inayotusumbua kila tunapokutana lakini tumejipanga kuhakikisha tunapata ushindi.
“Kwa sasa tumerejea kwenye ligi na lengo letu la kwanza ni kutetea ubingwa. Kuelekea mchezo wa kesho dhidi ya Mtibwa wachezaji wote wapo kamili hatuna majeruhi tunatarajia kupata ushindani mkubwa ingawa tumejiandaa kushinda,” amesema Matola.
Kwa upande wake Nahodha Msaidizi, Mohamed Hussein amesema ligi ilipofikia hatuangalii matokeo ya wapinzani ila kuhakikisha tunashinda kila mchezo ili kujihakikishia kutetea ubingwa.
“Sisi tunacheza mechi zetu, hatuangalii wengine wamefanya nini tunachotakiwa kufanya ni kushinda kila mchezo ili kutimiza malengo ya kutetea ubingwa,” amesema Matola.