Kikosi chetu kimeendelea kukusanya alama tatu kwenye Ligi Kuu ya Vodacom baada ya kuifunga Polisi Tanzania bao moja bila katika mtanange uliopigwa katika Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.
Katika mchezo huo hatukucheza kwa kasi kama kawaida yetu ambapo tulitengeneza nafasi kadhaa ambazo hatukuzitumia vizuri.
Luis Miquissone alitufungia bao hilo la pekee dakika ya 28 kwa mpira wa adhabu uliotinga wavuni moja kwa moja baada ya mlinzi mmoja wa Polisi kumfanyia madhambi Shomari Kapombe nje ya kidogo ya eneo la hatari.
Mshambuliaji Chris Mugalu alishindwa kuendelea na mchezo na kutolewa dakika ya 50 baada ya kupata maumivu ya mguu.
Kocha Didier Gomes aliwatoa Mugalu, Rally Bwalya na Mzamiru Yassin na kuwaingiza Medie Kagere, Erasto Nyoni na Hassan Dilunga.
Matokeo haya yanatufanya kufikisha pointi 70 na kuendelea kusalia kileleni mwa msimamo baada ya kucheza mechi 28.
Baada ya mchezo wa leo kikosi kitarejea jijini Dar es Salaam kujiandaa na mchezo ujao wa ligi dhidi ya Mbeya City utakaopigwa Jumanne, Juni 22 Uwanja wa Benjamin Mkapa.
One Response
Naipenda simba tokea niko tumboni mwa mama yangu