Safari yetu ya nusu fainali Afrika inaanza leo kwa Mkapa

Ni ndoto ya kila Mwanasimba kuiona timu yake ikitinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na leo saa tatu usiku safari yetu inaanza rasmi.

Kikosi chetu leo kinashuka katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuikabili Al Ahly katika mchezo mgumu wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mara kadhaa tumekuwa tukiishia hatua hii lakini sasa tunataka kuvunja mwiko na kutinga nusu fainali ingawa tunajua haitakuwa kazi rahisi.

Benchikha aweka wazi malengo ya timu….

Kocha Mkuu, Abdelhak Benchikha amesema pamoja na ubora na historia kubwa walionayo Al Ahly kwenye michuano hii lakini safari hii tumejipanga kuhakikisha sisi tunasonga.

Benchikha amesema tupo katika hali nzuri kwa sasa na tunaweza kushindana na timu yoyote na tutaingia katika mchezo wa leo kwa malengo ya kufanya vizuri ili kujiweka kwenye nafasi ya kufuzu nusu fainali.

“Timu iko tayari kwa ajili ya mchezo wa kesho, wachezaji wapo kwenye hali nzuri na tumepata muda wa kujiandaa kwa ajili ya kuwakabili Al Ahly.”

“Tunajua itakuwa mechi ngumu kwakuwa tunakutana na timu bora na yenye rekodi nzuri Afrika lakini tupo tayari kuwakabili,” amesema Benchikha.

Kapombe azungumza kwa niaba ya wachezaji…..

Mlinzi wa kulia, Shomari Kapombe amesema wapo tayari kwa ajili ya mchezo wa kesho na kila mmoja amejipanga kuhakikisha anaisaidia timu kupata matokeo chanya.

“Kwa upande wetu kama wachezaji tupo tayari kuipambania Simba kupata ushindi, tunajua haitakuwa mechi rahisi lakini tumejipanga na lengo ni kutinga nusu fainali,” amesema Kapombe.

Chama arejea…..

Kiungo mshambuliaji Clatous Chama amerejea kutoka nchini kwao Zambia na jana jioni amefanya mazoezi ya mwisho na wachezaji wenzake.

Chama alikuwa kwenye majukumu ya timu yake ya Taifa ya Zambia ‘Chipolopolo’ na juzi Jumaane aliiwezesha kupata ushindi mabao 2-1 dhidi ya Malawi.

Ujumbe kwa mashabiki…..

Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu, Ahmed Ally amewaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi uwanjani ili kuipa sapoti timu na anaamini kujitokeza kwao wingi kutakuwa msaada mkubwa na kuipeleka timu nusu fainali.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER