Robertinho: Tumejipanga kuingia hatua ya makundi kesho

Licha ya kutegemea kupata upinzani mkubwa kutoka kwa Power Dynamos katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika utakaopigwa kesho Azam Complex saa 10 jioni Kocha Mkuu, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amesema tumejipanga kuhakikisha tunashinda na kuingia hatua ya makundi.

Robertinho amesema timu imepata muda wa kujiandaa na wachezaji wapo kwenye hali nzuri kuhakikisha tunapata matokeo ya ushindi yatakayotuvusha.

Akizungumzia kukosekana kwa mlinzi wa kati, Henock Inonga katika mchezo wa kesho Robertinho amesema “Henock ni beki bora sio Tanzania tu bali Afrika, tutamkosa kesho lakini tayari tumemuandaa mbadala wake na ninaiamini timu yangu.”

“Mara zote kocha anahitaji kuwa na wachezaji wake bora lakini katika mpira hili linatokea hata wenzetu Power Dynamos watawakosa wachezaji wao watatu,” amesema Robertinho.

Kwa upande wake kiungo mshambuliaji, Clatous Chama amesema kila mchezaji anajua umuhimu wa mchezo wa kesho na yupo tayari kuipigania timu kuhakikisha tunaingia hatua ya makundi.

“Sisi wachezaji tunajua umuhimu wa mchezo wa kesho, tunafahamu furaha ya mashabiki wetu inatutegemea kwahiyo tutajitoa kuhakikisha hilo linatokea ingawa tunajua tutapata upinzani mkubwa,” amesema Chama.

Katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliopigwa Ndola; Zambia kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa tulitoka sare ya mabao 2-2.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER