Robertinho: Tumejiandaa kwa ushindi dhidi ya Raja Kesho

Kocha Mkuu, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amesema licha ya ukubwa na historia iliyonayo Raja Casablanca katika soka la Afrika lakini tumejipanga kuhakikisha tunapata ushindi katika mchezo wetu wa nyumbani.

Robertinho amesema mpira ni mchezo wa nyakati ukiwa bora kwa wakati huo unaweza kupata ushindi bila kujalisha unacheza na timu gani.

“Kila mechi kwenye michuano hii ni ngumu, tunaiheshimu Raja ni timu nzuri na ina historia kubwa katika soka la Afrika lakini malengo yetu ni kuhakikisha tunashinda nyumbani.

“Simba ni timu kubwa na malengo yake ni kufika mbali ikiwezekana hata kuchukua ubingwa lakini ili iwezekane inapaswa kuanzia kwenye hatua hii.”

Akizungumzia kukosekana kwa kiungo mkabaji Sadio Kanoute kutokana nakutumikia adhabu ya kadi tatu za njano Robertinho amesema:

“Sadio ni mchezaji muhimu wa kikosi cha kwanza lakini Simba imesajili wachezaji zaidi ya 28 na tulivyoenda kambini Dubai tuliwaandaa wachezaji kila nafasi wawili na kila atayepata nafasi atakuwa tayari kuipigania timu, tunahitaji ushindi,” amesema Robertinho.

Kwa upande wake nahodha, John Bocco amesema wamepata maandalizi mazuri na kila mmoja yupo tayari kupambana kuhakikisha tunashinda.

Akizungumzia kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano Dk. Samia Suluhu Hassan ya kutoa kitita cha Sh. 5,000,000 kwa kila goli tutakalofunga Bocco amesema:

“Ni kitu cha kipekee kwetu wachezaji kupokea kauli ya Rais, ameonyesha anatujali na tumeichukua kama morali na tunamuahidi hatutamuangusha, hii sio kwa Simba tu bali ni Watanzania wote,” amesema Bocco.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER