Kocha Mkuu, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amefurahishwa na usajili wa kikosi pamoja na benchi jipya la ufundi lililosukwa kuelekea msimu mashindano 2023/24.
Robertinho amesema wachezaji wanaoendelea kusajiliwa pamoja na wale waliopo wanatengeneza kikosi imara ambacho anaamini kitatupa mataji msimu ujao.
Robertinho ameongeza kuwa kwa sasa kila nafasi ina wachezaji bora kuanzia wawili kitu ambacho kitakuwa msaada mkubwa msimu ujao.
“Nimeridhika na kikosi changu, wachezaji wapya wanaosajiliwa ni wazuri hata wale waliopo wako imara. Tunaamini maandalizi yetu yatakuwa mazuri nchini Uturuki.
“Kuna wachezaji wengine wapya tutaungana nao tukiwa Uturuki kukamilisha kikosi. Msimu ujao tunahitaji kucheza vizuri na kushinda mataji, Simba ni timu kubwa na hilo lipo ndani ya uwezo wetu,” amesema Robertinho.
Kuhusu benchi jipya la ufundi Robertinho amesema “makocha wote walioletwa wana wasifu mzuri, wana vigezo vyote vilivyoidhinishwa na Mamlaka naamaini tutafanya kazi nzuri.”