Kocha Mkuu, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amesema kesho hatutacheza dhidi ya Wydad Casablanca kama ilivyokuwa kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza uliopigwa wiki iliyopita katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Robertinho amesema kesho tutakuwa ugenini kwa hiyo tutaingia na mbinu tofauti za kucheza aina hiyo mchezo haiwezi kuwa sawa na ile ya mkondo wa kwanza.
Robertinho ameongeza kuwa lengo letu litakuwa ni lile lile kucheza vizuri na kupata ushindi ili tufuzu hatua ya nusu fainali.
“Tumejiandaa na mbinu tofauti za kucheza mchezo wa kesho wa maruadiano wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wydad.
“Haiwezi kuwa sawa na vile tulivyocheza mechi ya kwanza ya nyumbani, nawaamini wachezaji wangu watafuata maelekezo tuliyowapa. Tumejipanga kucheza vizuri na kupata ushindi,” amesema Robertinho.
Kwa upande wake kiungo mshambuliaji, Pape Sakho amesema wachezaji wako tayari kimwili na kiakili kupambana kuhakikisha tunatimiza malengo.
“Sisi wachezaji tupo tayari, tumepata maandalizi ya kutosha, tupo tayari kukamilisha kazi tuliyoianza wiki iliyopita tukiwa nyumbani,” amesema Sakho.