Kocha Mkuu, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amesema tulikosa bahati katika mchezo wetu dhidi ya Horoya na hilo limesababisha kupoteza ugenini kwa bao moja.
Robertinho amesema tumepoteza nafasi tatu za wazi tulizotengeneza ambazo tungetumia hata moja tusingepoteza mchezo.
Akizungumzia mchezo ulivyokuwa, Robertinho amesema wenyeji Horoya walikuwa bora kipindi cha kwanza lakini tulivyofanya mabadiliko cha pili tuliishika mechi ingawa hatukuzitumia nafasi tulizopata.
“Nadhani hatukuwa na bahati, tumepata nafasi tatu za wazi lakini tumeshindwa kuzitumia. Wenzetu wamepata moja wameitumia na huo ndio mpira.
“Tunarudi nyumbani kujiandaa na mchezo unaofuata dhidi ya Raja Casablanca, naamini wachezaji wetu wataitumia vizuri kupata ushindi nyumbani,” amesema Robertinho.
Mchezo wetu dhidi ya Raja utapigwa Februari 18 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.