Robertinho ataja sababu za kiufundi za kumuingiza Erasto jana

Kocha Mkuu Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amesema katika mchezo wa jana dhidi ya Vipers, kipindi cha pili ilibidi kumuingiza kiraka Erasto Nyoni ili kupoza mashambulizi baada ya Vipers kurudi kwa kasi.

Robertinho amesema Erasto ni bora kwenye kuituliza timu inaposhambuliwa pia anapiga pasi ambazo hazipotei na hilo lilimfanya kumuingiza na amesaidia timu.

Robertinho ameongeza kuwa kupata pointi tatu ugenini lilikuwa ndiyo jambo la kwanza bila kujali tumechezaje na amewapongeza wachezaji kwa kazi kubwa waliyofanya.

“Tuliingia kwa lengo la kutafuta alama tatu na tunashukuru tumefanikiwa kuzipata. Tulimuingiza Erasto kipindi cha pili ili kuituliza timu kutokana na kasi ambayo walirudi nayo Vipers kipindi cha pili,” amesema Robertinho.

Akizungumzia mechi ya marudiano ya nyumbani dhidi ya Vipers, Robertinho amesema tutahitaji kushinda pia ili kuzidi kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kuvuka hatua ya makundi.

“Ni jambo zuri kushinda nyumbani, jambo zuri itakuwa tunacheza mbele ya mashabiki wetu watakaokuja kutupa sapoti,” amesema Robertinho.

Tayari kikosi kimerejea salama jijini Dar es Salaam na wachezaji wamepewa mapumziko ya siku moja kesho watarudi mazoezini kujiandaa na mchezo wa hatua ya 16 bora wa Azam Sports Federation Cup (ASFC) dhidi ya African Sports utakaopigwa Alhamisi Uwanja wa Benjamin Mkapa.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER